WAAMUZI WAKUTANA NA RUNGU

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, (TPLB) katika kikao cha Agosti 26 ilipitia mwenendo wa matukio mbalimbali na kufanya maamuzi huku waamuzi wakifungiwa na wengine kupewa onyo.

Ni Raphael Ikambi aliyekuwa mwamuzi wa kati mchezo wa Coastal Union 0-2 Yanga uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Ikambi kwa mujibu wa taarifa ameondolewa kwenye ratiba za waamuzi kwa mizunguko mitatu.

Adhabu hiyo imetokana na kushindwa kutafsri vema sheria za mpira wa miguu kwa kushindwa kufanya maamuzi sahihi katika tukio la mchezaji wa Coastal Union, Mtenje Albano aliyemchezea mchezo hatarishi nyota wa Yanga, Yannick Bangala.

Pia mwamuzi wa kati Ahmada Simba aliyeamua mchezo wa Singida Big Stars 2-1 Mbeya City amefungiwa kwa kipindi cha miezi mitatu kutokana na kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu hasa katika tukio la adhabu ya mkwaju wa penalti iliyowapatia Singida Big Stars bao la kwanza dhidi ya Mbeya City.

Katika taarifa hiyo imeleza kuwa Klabu ya Yanga imetozwa faini ya shilingi laki tano kwa kosa la kufanya mabadiliko la wachezaji kwa mikupuoa minne badala ya mikupuo mitatu kama ilivyoanishwa kwenye kanuni.

Tukio hilo lilitokea kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union uliochezwa Agosti 20 pia mwamuzi wa akiba wa mchezo huo Abeid William kutoka Arusha na mwamuzi wa msaidizi namba moja Ferdinand Chacha kutoka Mwanza wamepewa onyo kali kwa kushindwa kusimamia vema na kutunza kumbukumbu za mabadiliko ya wachezaji.