WACHEZAJI STARS WAKATI MWINGINE KUJITOA

MCHEZO wa kwanza umekishwa na kila mmoja ameambulia maumivu hasa baada ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Uganda.

Haikuwa siku nzuri kwa mashabiki na wachezaji pia kutokana na malengo ambayo walikuwa wanatarajia kushindwa kutimia.

Uwanja wa Mkapa mbele ya mashabiki wao Stars ilikwama kuibuka na ushindi na mwisho wa mchezo ikapoteza jambo gumu kwa kila mmoja kuamini.

Ipo wazi kwamba wachezaji wameona namna walivyoweza kufanya makosa kwenye mchezo wao wa kwanza na sasa wanakwenda mchezo wa pili wa marudio.

Benchi la ufundi limeona namna kazi ilivyokuwa kwenye kulinda na kusaka ushindi ndani ya dakika 90 hilo nina amini litafanyia kazi kwa mechi ijayo.

Kukata tamaa kwa wakati huu inapaswa kuwa ngumu kwa sababu kwenye mpira lolote linaweza kutokea.

Ikiwa wao Uganda wameweza kushinda kwenye ardhi ya nyumbani inamaanisha kwamba wachezaji wana uwezo wa kushinda ugenini lakini ni mpaka waamue kujitoa kwa hali na mali.

Ukitazama namna Uganda walivyocheza mechi ile inaonyesha kuna jambo walikuwa wanalitafuta hivyo njia hiyohiyo inapaswa kutumika kwa mechi  ijayo kwa Stars kusaka ushindi.

Mchezo wa marudi utakuwa ni zaidi ya fainali kama wachezaji wa Stars wataamua kwa sababu watakuwa ugenini na wenyeji wao watakuwa wanahitaji ushindi kujihakikishia nafasi ya kufuzu kushiriki CHAN.

Kazi ni kwenu kwa wale watakaopata nafasi kupeperusha bendera ya Tanzania, haitakuwa kazi nyepesi lakini inawezekana wachezaji wakiamua kujitoa.

Kuundwa kwa benchi jipya haina maana kwamba ushindi unaweza kupatikana kirahisi ni lazima wachezaji kutimiza majukumu yao kwa kujituma bila kuchoka.