TAIFA STARS KAZINI LEO KUIKABILI UGANDA

KIM Poulsen, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo kuikabili Uganda.

Huu ni mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani, (CHAN), Uwanja wa Mkapa saa 10:00.

Poulsen amesema kuwa wanatambua Uganda ni moja ya timu ngumu inayohitaji umakini kwenye kupambana nao.

“Uganda tunawatambua hasa kwa namna ambavyo wanatumia nguvu kutafuta ushindi, utakuwa ni mchezo ambao unahitaji nguvu na akili kubwa kwenye kutafuta ushindi ila tupo tayari, muunganiko unazidi kuwa imara na unaona hata Shomari Kapombe naye amejumuishwa kwenye kikosi.

“Kiakili na mbinu tumejipanga ukizingatia wachezaji wametoka kucheza mechi za ligi hiyo inaongeza uimara, mchezo huu wa Uganda ni wa kwanza na mchezo wa pili ugenini utatupa picha ya sisi kuweza kufuzu CHAN ukichanganya na nguvu ya mashabiki basi kutakuwa na kitu cha kipekee,” amesema Poulsen.

Aishi Manula, nahodha msaidizi wa Taifa Stars amesema kuwa wanahitaji kufuzu CHAN na wachezaji wapo tayari kwa mchezo huo.

“Wachezaji tupo tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Uganda, ambacho tunahitaji ni kufuzu CHAN, benchi la ufundi limefanya kazi kubwa na tunawatambua Uganda na wao wanatujua pia,” amesema Manula.

Miongoni mwa wachezaji ambao wapo kwenye kikosi cha Stars ni pamoja na Jonas Mkude, Feisal Salum, Kibwana Shomari, Abdul Suleiman.