MAYELE ANATAKA TUZO LIGI KUU BARA

FISTON Mayele, mshambuliaji wa Yanga amebainisha kuwa malengo yake kwa msimu wa 2022/23 ni kutwaa kiatu cha ufungaji bora.

Nyota huyo msimu wa 2021/22 kasi yake ya kutupia mabao iligotea kwenye namba 16 na pasi nne.

Namba moja alikuwa ni staa wa Geita Gold, George Mpole ambaye alitupia mabao 17 na pasi nne za mabao.

Tayari Mayele ametupia mabao mawili kwenye ligi katika mechi mbili mfululizo ambapo aliwatungua Polisi Tanzania na Coastal Union bao mojamoja.

Nyota huyo amesema:”Msimu uliopita ulikuwa na ushindani mkubwa na nilikuwa ninajitahidi kuweza kutwaa tuzo ya ufungaji bora lakini haikuwezekana.

“Tumeanza msimu mwingine malengo ni kuona timu inapata matokeo mazuri nami kuona kwamba ninaweza kutwaa tuzo ya ufungaji bora kwa msimu huu licha ya kwamba haitakuwa kazi rahisi,”