Mohamed Salah Arejea Kikosi cha Kwanza Liverpool Baada ya AFCON

231115F_ WCQ_AMPSCC_Wm

Winga nyota wa Liverpool, Mohamed Salah, hatimaye amerejea kwenye kikosi cha kwanza cha klabu hiyo na kucheza mechi yake ya kwanza tangu alipokuwa akiitumikia timu ya taifa ya Misri katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Salah alianzishwa katika kikosi cha Liverpool kilichoibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Olympique Marseille ya Ufaransa, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa ugenini kwenye uwanja wa Stade Vélodrome.

Urejeo wa mshambuliaji huyo uliwashangaza mashabiki wengi duniani, ambao hawakutarajia kumuona tena uwanjani mapema, hali iliyotafsiriwa kama ishara ya wazi kuwa mvutano uliokuwepo kati yake na kocha Arne Slot umefikia tamati.

Katika mchezo huo, Salah alipata nafasi nzuri ya kufunga bao katika dakika ya 83, lakini hakufanikiwa kuitumia. Hata hivyo, Liverpool ilitawala mchezo kwa kiwango kikubwa, huku Dominik Szoboszlai akitajwa kuwa nyota wa mechi baada ya kiwango bora alichoonesha.

Awali, baadhi ya wachambuzi wa soka nchini England walihofia kuwa safari ya Mohamed Salah ndani ya Liverpool ingeweza kufikia mwisho mwezi Desemba, kufuatia kauli ya mchezaji huyo kwa vyombo vya habari akidai kuwa kulikuwa na watu ndani ya klabu ambao hawakumtaka, na kwamba alikuwa akilaumiwa binafsi kwa matokeo mabovu ya timu wakati huo.

Hata hivyo, kocha Arne Slot alithibitisha kabla na baada ya mechi hiyo kuwa tayari amemaliza tofauti zote na Salah, na akaeleza kuwa kurejea kwake kwenye kikosi cha kwanza ni sehemu ya mpango wa kurejesha matokeo chanya ndani ya klabu.

Kwa upande wake, Mohamed Salah aliripotiwa kuomba radhi kwa wachezaji wenzake, uongozi wa klabu pamoja na mashabiki, hatua inayotajwa kuzima kabisa mvutano uliokuwepo na kurejesha mshikamano ndani ya kikosi cha Liverpool.

Liverpool sasa inajiandaa kwa mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya England (Premier League) dhidi ya Bournemouth, wakisaka kuendeleza mwendelezo wa matokeo mazuri.