YANGA SC vs KVZ ni mchezo wa kwanza wa ushindani ndani ya mwaka mpya 2026 ambao umeanza na matukio ya michezo yakiendelea.
Ikumbukwe kwamba Januari 3 2025, Yanga SC chini ya Kocha Mkuu, Pedro Goncalves waliwasili salama Zanzibar kwa maandalizi ya mwisho mchezo wa leo Januari 4,2026.
Kocha huyo ameweka wazi kwamba wanaingia kwa tahadhari kubwa kwenye mchezo wa leo huku akiwakosa baadhi ya wachezaji muhimu.
Miongoni mwa wachezaji ambao watakosekana ni Djigui Diarrra kipa namba moja aliye katika majukumu ya timu ya taifa ya Mali iliyopo Morocco kwenye mashindano ya AFCON 2025 huku timu hiyo ikiwa imetinga hatua ya robo fainali.
Kocha huyo amesema: “Tunaanza rasmi mashindano haya na tumekuja kupambana kwelikweli. Tunakosa baadhi ya wachezaji wetu muhimu lakini bado tuna kikosi imara cha kushindana vilivyo.
“Tutatumia mashindano haya pia kuwapa nafasi wachezaji wetu wapya. Tunafahamu wanahitaji kujifunza falsafa zetu. Sio jambo rahisi, ni jambo ambalo linahitaji kukua hatua kwa hatua. Kupitia mashindano haya naamini vijana wetu wapya watatuonesha kile walicho nacho,” amesema Pedro.