Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi, wameitembelea Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” kambini jijini Cairo nchini Misri.
Waziri Kombo na Profesa Kabudi, wameitembelea kambi hiyo Desemba 17, 2025 na kuikabidhi bendera ya Taifa, ikiwa ni ishara ya kuitakia kila la kheri kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha michuano ya Kombe la AFCON huko nchini Morocco.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Kombo amewasihi vijana hao wachache kati ya wengi wa taifa hili kwa kutanguliza uzalendo kwanza na kuipigania bendera ya Taifa kwa jasho na damu ili kuliletea heshima taifa la Tanzania.

Kabudi, amekiahidi kikosi hicho ushirikiano wa kila aina katika kuhakikisha kikosi hicho kinafanya vyema katika michuano hiyo mikubwa na yenye heshima kubwa sio tu barani Afrika bali duniani kwa ujumla.
Pia Prof. Kabudi amewahimiza Watanzania kuipenda na kuipa moyo timu yao ya Stars kwa kuwashangilia na wale watakao kuwa na nafasi kwenda kujiunga nao kwenye mechi zao zote watakazocheza huko nchini Morocco.
Ikumbukwe kwamba kikosi cha Taifa Stars kipo kundi C lenye timu za Nigeria, Tunisia na Morocco na kikosi hicho kitaanza michuano hiyo kwa kucheza na timu ya Taifa ya Nigeria, Desemba 23,2025.