Klabu ya Yanga SC imetangaza rasmi kuwa itacheza mechi zake zote tatu za nyumbani katika hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.
Akizungumza kupitia taarifa rasmi ya klabu, Ofisa Habari wa Yanga SC, Ali Kamwe, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya uongozi kufanya tathmini ya kina na kuangalia maslahi mapana ya klabu katika kipindi hiki muhimu.
“Baada ya uongozi kufanya tathimini na kuangalia maslahi mapana ya Klabu yetu, nipende kuwatangazia kuwa mechi zetu zote tatu za nyumbani kwenye hatua ya makundi tutatumia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa klabu inawaomba mashabiki na wanachama wote kutoka visiwani Unguja na Pemba kujiandaa kikamilifu kuipokea timu, huku maandalizi yakiendelea kuelekea mchezo wao wa kwanza wa nyumbani dhidi ya FAR Rabat ya Morocco.
“Niwaombe sana mashabiki na wanachama wetu kutoka visiwa vya Pemba na Unguja kujiandaa kuipokea timu na maandalizi ya nguvu kuelekea mchezo wa kwanza wa nyumbani dhidi ya FAR RABAT,” ameongeza.
Kamwe pia ametoa wito kwa wanachama na mashabiki walioko mikoani kuendelea kuwaunga mkono wachezaji wao, akisisitiza kuwa umoja na mshikamano ndivyo vitakavyoiwezesha timu kufanya vizuri katika kundi hilo gumu.
“Wanachama wengine kutoka mikoani tujiandae pia, tupo kwenye kundi gumu lakini tukiwa wamoja, tukiendelea kushiriana kwa umoja wetu tutatoboa,” amesema Kamwe.
Klabu ya Yanga SC kwa sasa ipo kwenye maandalizi ya mwisho kuelekea hatua ya makundi, ambapo imepangwa kwenye kundi lenye timu ngumu kutoka Afrika Kaskazini na Kati, na inatarajia kuanza kampeni zake hivi karibuni.