Brendan Rodgers Ajiuzulu Celtic Scotland

Miamba ya soka ya Scotland, Celtic FC, imethibitisha kuwa Meneja wao Brendan Rodgers amejiuzulu rasmi leo kutoka nafasi yake ya ukocha.

Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na klabu hiyo, Celtic imesema imepokea na kukubali barua ya kujiuzulu kutoka kwa Rodgers, ambaye ataondoka katika majukumu yake mara moja.

“Brendan anaondoka Celtic tukiwa na shukrani kwa nafasi aliyochukua katika kipindi cha mafanikio endelevu ya klabu, na tunamtakia mafanikio zaidi katika siku zijazo,” imeeleza taarifa ya klabu hiyo.

Celtic imeongeza kuwa mchakato wa kuteua meneja mpya wa kudumu umeanza, na mashabiki watapewa taarifa zaidi mara tu utakapokamilika.

Katika kipindi hiki cha mpito, klabu imetangaza kuwa Martin O’Neill, aliyewahi kuwa meneja wa Celtic, pamoja na Shaun Maloney, mchezaji wa zamani wa timu hiyo, watasimamia masuala ya timu ya kwanza hadi meneja mpya atakapopatikana.

Taarifa hiyo pia imepongeza mchango wa Rodgers katika vipindi vyake viwili akiwa na Celtic, ambavyo vilishuhudia mafanikio makubwa kwa klabu hiyo ya kihistoria.