BAADA ya kutambulishwa ndani ya kikosi cha Simba SC kuwa mrithi wa mikoba ya Fadlu Davids, kocha mpya anatarajiwa kuwasili Bongo mapema Oktoba 4 2025.
Anaitwa Dimitar Pantev mwenye miaka 49 yeye ni raia wa Bulgaria ambaye alitambulishwa rasmi Oktoba 3 2025 kuwa ni kocha ndani ya kikosi hicho.
Kabla ya kutmbulishwa Simba SC alikuwa anafanya kazi katika timu ya Gaborone United iliyocheza na Simba SC katika hatua ya awali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo huo kwenye benchi Uwanja wa Mkapa kwa timu ya Simba SC alikuwa ni Hemed Morocco ambaye ni Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania.
Simba SC walimuomba kwa muda maalumu kwa ajili ya mchezo mmoja kwa sababu kocha msaidizi Seleman Matola alikuwa na kadi nyekundu kwenye mchezo wa kwanza ugenini hivyo hakuwa na vigezo kukaa kwenye benchi la ufundi.
Kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Mkapa baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba SC 1-1 Gaborone United, Simba SC ilitinga hatua ya pili kwa ushindi wa jumla mabao 2-1 kwa kuwa katika mchezo uliochezwa ugenini Simba SC ilipata bao 1-0 lililofungwa na Ellie Mpanzu.