Klabu ya Yanga SC imemtambulisha rasmi Romain Folz, kocha raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 35, kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo. Utambulisho huu unakuja baada ya aliyekuwa kocha, Miloud Hamdi, kutimkia klabu ya Ismaily ya nchini Misri.
Romain Folz, ambaye ni mzaliwa wa Bordeaux, Ufaransa, anakuja na wasifu mzito uliopambwa na uzoefu wa kimataifa na elimu ya juu ya ukufunzi. Ana shahada ya UEFA Pro Licence – leseni ya juu zaidi ya ukocha barani Ulaya – na pia amehitimu CONMEBOL Pro Licence, inayotambuliwa Amerika Kusini. Hili linamfanya kuwa mmoja wa makocha wachache barani Afrika waliobeba leseni mbili za kiwango cha juu kutoka mabara tofauti.
Uzoefu Wake wa Kiafrika
Kocha Folz si mgeni katika soka la Afrika. Amefundisha vilabu mbalimbali vikiwemo:
Horoya AC ya Guinea
AmaZulu FC ya Afrika Kusini,
Township Rollers ya Botswana.
Aidha, katika majukumu ya ukocha msaidizi, Folz aliwahi kufanya kazi na:
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini
Pyramids FC ya Misri
Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) – ambako alihusika katika maandalizi ya timu ya taifa kwenye mashindano ya kimataifa.