SIMBA SC YAREJESHA SHUKRANI, MIPANGO YAANZA

BAADA ya kupishana na mataji yote ndani ya msimu wa 2024/25, nahodha wa Simba SC, Mohamed Hussen Zimbwe Jr amerejesha shukrani kwa mashabiki na kubainisha kuhusu mipango ya msimu mpya wa 2025/26.

Mchezo wa mwisho kwenye Ligi Kuu Bara kwa Simba SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ilikuwa Juni 25 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga SC 2-0 Simba SC.

Ni taji la ligi, Kombe la Shirikisho Afrika Simba SC imegotea kwenye nafasi ya pili kwenye mashindano haya.Kwenye CRDB Federation Cup, Simba SC iligotea hatua ya nusu fainali ikifungashiwa virago na Singida Black Stars.

Ujumbe wa Zimbwe Jr na Simba SC upo namna hii:-“Kwanza, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu wa rehema kwa kutuwezesha kuanza ligi na kumaliza salama.

“Pili, uongozi chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji na makamu wake Murtaza Mangungu, benchi la ufundi, menejimenti, wanachama na mashabiki wote kwa kuwa bega kwa bega nasi mpaka mwisho wa msimu.

“Kwa mashabiki wetu, sijui nitumie maneno gani kuelezea shukrani zangu za dhati kwenu kwa mapenzi yenu makubwa kwetu. Hakika tuna deni la kulipa kwenu. I would never compare na kitu chochote kwenye suala la kutupa nguvu na kutupigania ndani na nje ya uwanja iwe kwenye jua kali au kwenye mvua mlikuwepo. Katika kila nyakati ngumu hamkukata tamaa, hamkutuacha. Mwenyezi Mungu awabariki sana. You are The True Heroes.

“Mwisho wa msimu mmoja ndio maandalizi ya msimu mwingine. Inshaallah next season tutafanya vizuri zaidi.”