Klabu ya Simba haikuhudhuria mkutano wa kabla ya mchezo (Pre-Match Conference) uliopangwa kufanyika leo Juni 24, 2025 saa 5:30 asubuhi na kuandaliwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Bodi hiyo, Karimu Boimanda, jitihada mbalimbali zilifanyika kuwasiliana na uongozi wa Simba, lakini hazikufua dafu. Mkutano huo ulikuwa sehemu ya maandalizi ya mchezo muhimu unaotarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Tumefanya jitihada zote, lakini hadi sasa hatujawapata. Kwa kuwa hili ni suala la kikanuni na kuna ratiba nyingine za kimchezo, tunatangaza rasmi kuwa mkutano umeahirishwa. Taarifa zaidi zitatolewa baadaye,” alisema Boimanda.
Aidha, Boimanda alibainisha kuwa Bodi itaendelea kufuatilia kujua sababu ya kutohudhuria kwa wawakilishi wa Simba SC, na itatoa taarifa rasmi endapo sababu hiyo itabainika.