JESHI LA POLISI LATOA ONYO KABLA YA MECHI YA WATANI WA JADI – VIDEO


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kuwa limechukua hatua kali za kiusalama kuelekea mchezo mkubwa wa soka kati ya timu ya Simba na Yanga utakaochezwa Jumatano, tarehe 25 Juni 2025, katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Akitoa taarifa kwa umma leo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro amesema vyombo vya dola kwa kushirikiana na wananchi, vinaendelea kuhakikisha kuwa hali ya usalama jijini inabaki kuwa shwari, huku tahadhari maalum ikielekezwa kwa tukio hilo la michezo linalovuta mashabiki wengi ndani na nje ya jiji.

Kamanda huyo amesisitiza kuwa hairuhusiwi mtu yeyote kufika uwanjani na silaha ya aina yoyote, isipokuwa askari maalum waliopangwa kwa ajili ya kulinda amani. Aidha, magari yatakayoingia uwanjani ni yale tu yenye vibali maalum vilivyotolewa na mamlaka husika.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa mashabiki wa soka kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani kabla, wakati na baada ya mechi hiyo maarufu ya watani wa jadi, ikisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayevuruga amani au kuvunja sheria.

“Jeshi la Polisi Kanda Maaalum ya Dar es Salaam linatoa wito kwa wapenda soka wote kujiepusha na vitendo visivyo vya kiungwana kabla, wakati na baada ya mchezo huo,” amesema Kamanda Muliro.