Katika mfululizo wa matukio makubwa yanayoikumba Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Steven Mnguto amejiuzulu rasmi nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi, huku Ofisa Mtendaji Mkuu, Almasi Kasongo, akisimamishwa kazi na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia.
Taarifa ya Juni 13 iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, imeeleza kuwa barua ya kujiuzulu kwa Mnguto imepokelewa rasmi, na kusimamishwa kazi kwa Kasongo ni hatua nyingine katika msururu wa mabadiliko ndani ya uongozi wa TPLB.
Tukio hili limeibua hisia kali kutoka kwa wadau mbalimbali wa michezo, wakiwemo wanahabari na wachambuzi. Mwandishi mkongwe wa michezo, Saleh Ally maarufu kama Saleh Jembe, ameandika kwa uchungu na tahadhari kupitia mitandao ya kijamii:
“Steven Mguto ameenda, Almasi Kasongo amesimamishwa na wengi imekuwa furaha kuu. Kosa lao? Hii itabadilisha nini katika soka letu? Kwa faida ya nani?”
Akiendelea kwa hisia nzito, Saleh ameonya kuhusu siasa ya michezo akisema:
“Siasa ya soka imewaondoa lakini si mwisho kwao. Tukubali, hawana kosa wala hatia. Na kama tunaamini dhulma ni jambo sahihi, basi tukumbuke: Dhulma hurejea… Nitawakumbusha.”
Kauli hizo zimeibua mjadala mpana miongoni mwa wadau wa soka, huku baadhi wakipongeza hatua hizo wakiamini ni mwanzo wa mageuzi, ilhali wengine wakionya kuwa huenda kuna ajenda zisizo rasmi nyuma ya pazia.