SAKATA LA MECHI YA YANGA NA SIMBA LATINGA BUNGENI, SERIKALI YATOA KAULI

Sakata la mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na Simba limechukua sura mpya, baada ya kutinga bungeni, huku serikali kuombwa itoe kauli kuhusu kinachoendelea.

Suala hilo liliibuliwa asubuhi leo Juni 11, 2025 na Mbunge wa Makete, Festo Sanga kwenye swali lake la nyongeza kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, akiomba kauli ya serikali kuhusu mvutano unaoendelea wa miamba hiyo miwili ya soka nchini.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema michezo ukiwemo mpira wa miguu una mamlaka zake, ambazo zinasisitiza serikali kutoingilia moja kwa moja mamlaka hizo ili kuepuka kufungiwa na kuzitaja mamlaka hizo kuwa ni Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Bodi ya Ligi (TPLB) na Shirikisho la Kimataifa kla Mpira wa Miguu (Fifa).

Hata hivyo amesema serikali inafuatilia kwa karibu kuhusu mgogoro wa mchezo huo, ambao awali ulipangwa kuchezwa Machi 8, 2025 na sasa umepangwa kuchezwa Juni 15, 2025 na kwamba TFF na TPLB zifuate kanuni na taratibu ilizojiwekea.

“Kama unavyofahamu shughuli za mpira wa miguu zina mamlaka yake kitaifa na za kimataifa na tumekuwa tukisisitizwa mara kwa mara serikali kutoingilia moja kwa moja uendeshaji wa shughuli hizo, ili kuepuka pengine hata kufungiwa na Fifa nyakati hizi ambazo kitakwimu nchi yetu inafanya vizuri katika shughuli za uendeshaji wa mpira wa miguu.

“Kuhusu mchezo anaousema tunafuatilia kwa karibu unavyoendelea kutatuliwa, lakini huku tukijaribu kwa kiwango kikubwa kutoingilia moja kwa moja maamuzi ya TFF na Bodi ya Ligi,” amesema Naibu Waziri.