Klabu ya Yanga imejibu mapigo baada ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kudai klabu hiyo fedha zao za zawadi katika mashindano mbalimbali zikatwe kulipia malipo wanayotakiwa kuilipa kwa TFF huku ikidai kuwa haijawahi kulipwa fedha yoyote ya Ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa Misimu mitatu mfululizo, (2021/2022, 2022/2023 na 2023/24).
Taarifa ya leo Juni 10, 2025 iliyotolewa na klabu hiyo imeeleza taarifa ya TFF Madai hayo imeshindwa kufafanua deni lenyewe na kubainisha kuwa TFF wamekuwa wakishikila fedha hizi za Ubingwa kwenye akaunti zao kila Msimu unapomalizika huku wakifahamu ni makosa na ni kinyume cha utaratibu.
Yanga Sc imesema hakuna uthibitisho wowote wa kimaandishi kuonyesha kama TFF wamewahi kulipa fedha hizo za Ubingwa kwa Klabu ya Yanga na na kusisitiza kuwa ni aibu na fedheha na kumtia dosari mdhamini kuendesha mashindano bila kumlipa Bingwa kwa misimu mitatu mfululizo.
“Tunaelekeza, dawa ya deni ni kulipa kwa wakati ikiwa ni haki ya mshindi na inampa heshima mdhamini wa mashindano. leleweke, ada za malipo ya wachezaji wa kiger kigeni walizozisema kwenye taarifa yao hulipwa mwanzo wa msimu mpya na hela hizi za Ubingwa hutolewa Mwisho wa msimu.” — imesema taarifa ya Yanga Sc.
“Klabu ya Young Africans haijawahi kupokea taarifa yoyote rasmi kutoka TFF kuhusu Klabu yetu kuwa na deni kwao. Uongozi wa Klabu ya Young Africans unaendelea kusisitiza kulipwa pesa yake ya Ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB, kwa msimu wa 2023/24 ili tuweze kucheza mchezo wa Fainali siku ya tarehe 28 Juni, 2025.” — imesema Yanga Sc