Shirikisho la soka Tanzania (TFF) imetoa ufafanuzi kuhusu Madai ya klabu ya Yanga Sc kuhusu kutolipwa zawadi ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB ya Tsh milioni mia mbili (200,000,000) kubainisha kuwa TFF ndiyo inayoidai klabu hiyo ikiwemo malipo ya ada za wachezaji wa kigeni.
Taarifa ya leo Juni 10, 2025 ilitolewa na TFF imeeleza kuwa msimu wa 2023/2024 wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB (CRDB Bank Federation Cup), benki hiyo ililipa fedha zote za kimkataba Tsh. 255,000,000/= kwa ajili ya uendeshaji wa mashindano hayo.
Aidha TFF imebainisha kuwa klabu ya Yanga iliomba kwa barua fedha zao za zawadi katika mashindano mbalimbali zikatwe kulipia malipo wanayotakiwa kulipa kwa TFF ikiwemo ada za wachezaji wa kigeni hatua inayokuja baada ya Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Sc kudai klabu hiyo inaidai TFF Tsh milioni 200
kama zawadi ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB.
“Tunapenda kutoa ufafanuzi kuwa TFF ndiyo inayoidai klabu hiyo. Young Africans SC iliomba kwa barua fedha zao za zawadi katika mashindano mbalimbali zikatwe kulipia malipo wanayotakiwa kulipa kwa TFF ikiwemo ada za wachezaji wa kigeni.”— imesema sehemu ya taarifa ya TFF.
“Hivyo, ili kutoendelea kusababisha sintofahamu kwa umma, tumeiandikia barua Young Africans kutuma kwetu mtaalamu wao wa fedha kesho saa 4 asubuhi kuhakiki deni la klabu hiyo akiwa na vielelezo vyote katika Ofisi za TFF.”— imesema TFF.