MAAZIMIO MANNE YA YANGA SC YAPO NJE YA UWEZO WA BODI

ALMAS Kasongo, CEO wa Bodi ya Ligi Tanzania ameweka wazi kuwa maazimio manne ambayo Yanga SC wamepeleka kwenye kikao walichokaa yapo nje ya uwezo wa bodi hivyo watapeleka kwenye mamlaka husika ili yafanyiwe kazi.

Ikumbukwe kwamba Juni 9 2025 kulikuwa ni kikao maalumu kati ya Bodi ya Ligi Tanzania na Yanga SC kilichofanyika makao makuu ya Bodi ya Ligi, Ilala, Dar Tanzania na miongoni mwa jambo ambalo lilijadiliwa ni kuhusu mchezo wa Kariakoo Dabi ambao umepangwa kuchezwa Juni 15 2025 huku Yanga SC wakibainisha kuwa hawapo tayari kucheza mpaka matakwa yao manne yafanyiwe kazi.

Kasongo amesema: “Wenzetu wamekuja na mambo manne ambayo sisi kama bodi tuna wajibu wa kupokea na kuyachakata, sio kupokea tu na kuyachakata. Azimio la kwanza kuvunjwa kwa kamati ya usimamizi na uendeshaji ya bodi ya ligi. Kuna kamati ya kusimamia na kuendesha ligi ipo kwenye kanuni.

“Jambo la pili kujiuzulu kwa ofisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, jambo la tatu kujiuzulu kwa katibu Mkuu wa TFF na jambo la nne bodi ya ligi iwe chombo huru.

“Itoshe kusema kuwa tumepokea lakini haya mambo yote manne yapo nje ya uwezo wa Mwenyekiti wa Bodi, mamlaka ya utendaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu ndio wana uwezo kuyafanyia kazi na tutapeleka kwenye mamlaka husika.

“Kama nilivyotangulia kusema kwa haya waliyoyaleta tumeyapokea ila yapo nje ya uwezo wetu tuna mamlaka ya kuwasilisha kwa mamlaka inayohusika ili kuyafanyia maamuzi.

“Kwa yale ambayo yapo ndani ya uwezo wetu ikiwa ni ratiba sisi ratiba yetu ipo kama ilivyopangwa kwa sababu chombo kinachoendesha na kusimamia ligi ni chombo kingine.

“Ratiba yetu tulisema kuwa mechi namba 184 itachezwa Juni 15 2025, sisi tuna wajibu kupeleka hoja katika mamlaka husika, ratiba ipo vilevile mpaka kamati itakapotoa taarifa nyingine.

“Yanga SC nafasi yao ni kwamba wangetamani haya yafanyike ili warudi kwenye mchezo, ukitazama haya yanawezekana lakini haitakuwa kwa siku moja ni mchakato ambao unahusisha kamati nyingi. Ukiyatazama maazimip yapo nje ya mamlaka ya bodi ya ligi.”

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu itazinduliwa rasmi Julai 24 2025 usipange kukosa.