SIMBA SC imekamilisha dakika 90 za mwanzo Uwanja wa Amaan kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali Kombe la Shirikisho Afrika kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini.
Bao pekee la uongozi limefungwa na Jean Ahoua kwa pigo la faulo dakika ya 45 akitumia mguu wake wa kulia. Kwa matokeo ambayo yamepatikana Uwanja wa Amaan na Simba SC wakiwa nyumbani ni mtihani mzito ugenini kulinda kwa kuwa walitinga hatua ya nusu fainali kwa kupindua meza mbele ya Al Masry.
Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wa ugenini ubao ulisoma Al Masry 2-0 Simba na ule uliochezwa Uwanja wa Mkapa ilikuwa Simba 2-0 Al Masry na Simba ikashinda kwa penati kwa maana hiyo mashindano ya kimataifa kila mtu mbabe nyumbani.
Mchezo wakukamilisha dakika 90 ugenini Simba wanakazi kutafuta ushindi mwingine ikiwa wataruhusu kufungwa bao kwa kuwa walitengeneza nafasi zaidi ya tano wakatumia moja.
Ahoua alikosa nafasi mbili za wazi akiwa ndani ya 18 dakika ya 49 kwa pigo la kichwa baada yakupigiwa krosi na Steven Mukwala na dakika ya 90 akiwa ndani ya 18 baada ya kupigiwa pasi na Mpanzu.
Kwenye eneo la kiungo Simba bado haijawa imara huku wapinzani wao Stellenbosch FC wakionekana kuwa na nguvu zaidi kwenye kujilinda.