Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa maamuzi tofauti kwa maofisa habari wa vilabu vya Yanga na Simba baada ya kupitia mashauri yaliyowasilishwa mbele yake.
Katika kikao chake cha kupitia mashauri hayo, Kamati hiyo ilimkuta na hatia Ali Kamwe, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, kwa kosa la kuchochea umma kinyume na Kanuni ya 73(4) ya Kanuni za Maadili ya TFF, Toleo la mwaka 2021. Shtaka hilo liliwasilishwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi.
Baada ya kusikiliza pande zote na kupitia vielelezo husika, Kamati ilimhukumu Kamwe kulipa faini ya shilingi milioni tano (5,000,000) na kumpa onyo kali la kutofanya kosa la kimaadili ndani ya kipindi cha miaka miwili. Adhabu hiyo imeanza kutekelezwa rasmi kuanzia tarehe 16 Aprili 2025.
Kwa upande mwingine, Kamati hiyo hiyo haikumkuta na hatia Ahmed Ally, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba SC, ambaye alishtakiwa na klabu ya Yanga kwa tuhuma kama hizo – kuchochea umma kinyume na Kanuni 73(4) ya Kanuni za Maadili ya TFF.
Katika hukumu yake, Kamati ilieleza kuwa baada ya kupitia hoja na vielelezo kutoka pande zote, haikupatikana ushahidi wa kutosha kuthibitisha kosa dhidi ya Ahmed Ally, hivyo ikamuachia huru.