FA: SIMBA KUPUNGUZA MAJUKUMU, UBINGWA INAWEZEKANA

 NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kama FA ambaye alikuwa ni mgeni rasmi kwenye Jambo Kubwa Kuliko East and Central Africa Aprili 16 2025 amesema kuwa ikiwa yaliyosemwa yatakuwa kwenye utekelezaji yataleta matokeo mazuri na kupunguza matumizi kwenye baadhi ya masuala ya viwanja.

Mwinjuma amesema kuwa anaamini Simba SC ina nafasi yakutinga hatua ya fainali kwa kupata matokeo nusu fainali ya kwanza na ile itakayochezwa Afrika Kusini.

“Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu imewekeza sana kwenye michezo na hasa mchezo huu pendwa wa mpira wa miguu. Ki takwimu hakuna kipindi tumefanya vizuri kama kipindi hiki. Mchezo huu unaendelea kutupa raha mioyoni na kututangaza nje ya mipaka ya nchi.

“Hili nililosikia leo la ujenzi wa uwanja limenivutia sana. Mkiwa na kiwanja cha watu 10,000 au 12,000 kinaweza kutumika kwa michezo ya ndani, michezo ya nje ndio mkawa mnatumia Uwanja wa Mkapa, mtaupunguzia hata majukumu.

“Itoshe kusema ni uwekezaji wa mkakati ambao umekuja wakati sahihi. Serikali kama mlezi wetu tunawapongeza sana. Naamini mna maarifa ya kucheza mchezo wa nusu fainali utakaochezwa Zanzibar na kule Afrika Kusini na kuhakikisha mnavuka na kuingia fainali hadi kushinda ubingwa wa Afrika. Na sisi kama serikali kama mara zote ambavyo tunawaunga mkono hatutawaacha hata wakati huu. Tupo nyuma yenu kuhakikisha mnashinda ubingwa wa Afrika. Hatuishii Hapa.”