WABABE wawili ndani ya Ligi namba nne kwa ubora Afrika, Fountain Gate ambayo Ofisa Habari wao ni Issa Mbuzi na Yanga Ofisa Habari ni Ali Kamwe wanatarajia kukutana Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Aprili 21 2025 kwenye mchezo wa ligi ambao ni mzunguko wa pili.
Rekodi zinaonyesha kwamba Fountain Gate ni namba mbili kwa timu ambazo zimeruhusu mabao mengi ndani ya ligi ambayo ni 47 baada yakucheza mechi 26 ikiwa nafasi ya 9 na pointi zake kibindoni ni 29 inakwenda kuwakaribisha Yanga ambao ni namba moja kwenye eneo la utupiaji.
Safu ya ushambuliaji ya Fountain Gate imefunga jumla ya mabao 29 ilipata ushindi kwenye mechi 8 huku ikipoteza 13 nakuambulia sare 5 kwenye hizo sare miongoni waliwabana mbavu watani wa jadi wa Yanga, Simba ubao uliposoma Fountain Gate 1-1 Simba.
Katika dakika 2,340 ni wastani wa kila dakika 80 kufunga bao na kila baada ya dakika 49 timu hiyo ina wastani wakuokota mpira kwenye nyavu zake ndani ya mechi za ligi msimu wa 2024/25.
REKODI ZA YANGA
Yanga ni vinara ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya mechi 25 ni pointi 67 wamekusanya kibindoni na safu ya ushambuliaji imetupia jumla ya mabao 64 ikiwa ni safu kali kwenye kumalizia nafasi ambazo zinatengenezwa ndani ya uwanja kwenye ligi.
Kwenye dakika 2,225 ina wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 35 huku ukuta ukiwa na wastani wakuokota bao nyavuni kila baada ya dakika 225 kwenye mechi za ushindani wakiwa uwanjani kutimiza majukumu yao.
Ukuta wake ni namba mbili ndani ya ligi kuruhusu mabao machache ambayo ni 10, timu namba moja kwenye ligi ambayo imeruhusu mabao machache zaidi kwa sasa ni Simba ikiwa imetunguliwa mabao 8 na yote aliyetunguliwa ni kipa Moussa Camara.
Yanga ilipata ushindi kwenye mechi 22, ilikubali sare dhidi ya JKT Tanzania 0-0 Yanga na mechi mbili ilipoteza dhidi ya Azam FC na Tabora United. Wababe hawa wawili ambao walikomba pointi tatu dhidi ya Yanga kwenye mzunguko wa pili walilipa kisasi.
Yanga ilipokutana na Tabora United ugenini ilipata ushindi wa mabao 3-0 na ilipokutana na Azam FC ilipata ushindi wa mabao 2-1. Ni mchezo wao wa ligi dhidi ya Azam FC waliruhusu bao moja langoni akiwa Djigui Diarra ambaye ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Miloud Hamdi.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.