HAWA HAPA WAPIGAJI PENATI SIMBA, CAMARA ATIMIZA MAJUKUMU

KIKOSI cha Simba chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids, Aprili 9 2025 kiliandika rekodi ya kutinga hatua ya nusu fainali Kombe la Shirikisho Afrika kwa ushindi wa penati 4-1 baada ya dakika 90 za pili ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 2-0 Al Masry.

Fadlu kabla ya mchezo aliweka wazi kuwa mpango mkubwa ni kupata ushindi na kuzuia kutofungwa ndani ya dakika 90 jambo ambalo wachezaji walitimiza kwa ushirikiano ndani ya dakika 90, safu ya ulinzi chini ya Hamza Jr ilifanya kazi kubwa kwa ushirikiano na Zimbwe Jr ambaye ni nahodha, Shomari Kapombe Legend wa muda wote Simba.

Katika dakika 45 za mwanzo Simba waliwanyanyua mashabiki wao kupitia kwa Ellie Mpanzu dakika ya 22 na Steven Mukwala dakika ya 32 na ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wa robo fainali ya kwanza Uwanja wa Suez Canala ulisoma Al Masry 2-0 Simba hivyo mshindi alitafutwa kwa penati.

Mukwala alipachika bao la pili kwa pigo la kichwa akitumia krosi iliyotoka kwenye mguu wa beki wakupanda na kushuka Mohamed Hussein Zimbwe Jr ambaye alikuwa kwenye majukumu yake kama Camara ambaye alifanya kazi yake kuzuia mpira usiguse nyavu za Simba.

Kwa upande wa Simba mpigaji wa kwanza wa penati alikuwa ni Jean Ahoua, penati ya pili mpigaji alikuwa ni Steven Mukwala, penati ya tatu mpigaji alikuwa ni Kibu Dennis na penati ya nne ya maamuzi ilipigwa na Shomari Kapombe, wapigaji wote wa Simba walifunga kwa kutumia mguu wakulia, huku Moussa Camara kipa wa Simba akiokoa penati mbili kati ya tatu ambazo walipiga Al Masry.

Mlinda mlango wa Al Masry, Gad hakuwa na bahati kwenye mchezo huo kwa kuwa wapigaji wa Simba walifunga penati zote walizopiga huku Camara akiokoa mbili na moja ilizama mazima nyavuni.

Simba inatinga hatua ya nusu fainali na mchezo ujao wa hatua hiyo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa itakuwa dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini Aprili 20 na kete ya pili itamaliziwa ugenini Aprili 27, Afrika Kusini.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.