KUNA nyakati marafiki walikosa chakula na mfukoni hawakuwa na hata mia mbovu, ilikuwa vita ngumu kwao kupita kwa wakati huo ila waliibuka mashujaa bila kutarajia katika nyakati hizo kutokana na zile stori ambazo walianza kupiga.
Ghafla waliacha kuzungumzia kuhusu bili waliyoacha kwa mama Amina pamoja na yale madeni ambayo yapo juu yao kwenye lile daftari la kudumu la yule mangi wa mtaa wao ambao hakuwa na jambo dogo kwenye suala la kudai chake.
Stori za kurudishwa nyumbani kwa kukosa ada hizo walisahau, unajua walikuwa wanazungumza kuhusu nini wakati huo? Ilikuwa ni namna watakavyotesa kwa kula vyakula vizuri pindi watakapopata fedha walizokosa wakati wakiwa na njaa.
Hizo stori zilipigwa mchana mpaka jioni hakuna aliyefikiria kwamba wamekosa chakula bali hesabu zao ilikuwa wakipata fedha lazima wale kile wanachohitaji na sio kile wanachokipata, hivyo tu kesi yao ikafungwa.
Unakumbuka ndani ya kikosi cha Yanga kuna beki wa kazi ambaye alikuwa akipewa penati kupiga anapaisha na wenzake wakiwa kwenye stori wanamkumbusha jambo hilo lakukosa penati.
Mwamba kwenye mchezo mmoja wa ligi uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Yanga walipopata penati iliyosababishwa na Jean Baleke alionekana kutaka kuipiga penati hiyo mpaka nahodha Bakari Nondo alipomuondoa kwenye eneo hilo.
Unajua Nondo alipohojiwa kwa nini alimzuia beki huyo kupiga penati jibu lake lilikuwa ni nini? Alijibu kwa utani akiwa na furaha kwamba nilimwambia tukikupa upige penati tunaweza okota mpira Nungwi, kesi ikaisha.
Ni Ibrahim Bacca, beki wa kazi ambaye kwenye eneo la ukabaji yupo imara na akipewa jukumu hilo la kuanza ama aanzie benchi lazima utafurahia utendaji wake kazi kwa umakini mkubwa ndani ya uwanja.
Rekodi zinaonyesha kuwa msimu wa 2022/23 beki huyo alipata nafasi yakucheza mechi 11 za ligi akikomba dakika 761, hakuingia kwenye orodha ya nyota waliofunga bao wala kutoa pasi kulingana na eneo ambalo yupo kwenye majukumu yake na Yanga ilitwaa ubingwa wa ligi.
Katika mchezo wake wa kwanza msimu wa 2022/23 alikomba dakika 90 mazima ilikuwa dhidi ya KMC mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa ilikuwa ni Oktoba 26 2022 na pilato wa mchezo alikuwa ni Elly Sasii.
Katika mchezo huo baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 1-0 KMC, pointi tatu zilikuwa mali ya watoto wa Jangwani mazima. Bacca alipewa majukumu ya kupiga faulo alifanya hivyo dakika ya 12, 29, 44 na 48.
Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba walipocheza na Kagera Sugar 0-1 Yanga aliingia kwenye orodha ya wachezaji walioonyeshwa kadi ya njano na mwamuzi Ramadhan Mwinyimkuu ilikuwa dakika ya 63 baada ya kucheza faulo na aliokoa hatari dakika ya 6, 48, 60, 76.
2023/24 ni mechi 21 alicheza ambapo hapo alikuwa amejenga ushikaji na kikosi cha kwanza akitibua rekodi ambayo aliiweka msimu uliopita kwa kukomba dakika chache uwanjani. Msimu wa 23/24 alisepa na dakika 1,788.
Mchezo wake wa kwanza kwenye ligi ilikuwa dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa Azam Complex na mwamuzi alikuwa ni Shomari Lawi mchezo ulichezwa Agosti 23 2023 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 5-0 KMC Complex.
Katika mchezo huu Bacca alikomba dakika 90 mazima na Yanga iliandika rekodi yakupata ushindi mkubwa kwenye mchezo wa kwanza na mwisho wa msimu walitwaa taji la ligi.
Kama ambavyo aliingia kwenye orodha ya wachezaji walionyeshwa kadi ya njano kwenye mchezo wa msimu wa 2022/23 dhidi ya Kagera Sugar, rekodi hiyo ilijirudia tena kwa mara nyingine msimu wa 2024/25 ambapo kwenye mchezo uliochezwa Azam Complex alikutana nacho.
Ilikuwa ni Mei 8 2024 dakika ya 88 beki huyo alionyeshwa kadi ya njano na mwisho ubao ulisoma Yanga 1-0 Kagera Sugar, pointi tatu zilikuwa ni mali ya Yanga.
Kwa msimu wa 2024/25 beki huyo ameandika rekodi mpya kwa kuwa beki namba moja mwenye mabao mengi ndani ya ligi akifikisha mabao manne kibindoni na katika mabao hayo kuna bao la mkono wa maajabu alifunga dhidi ya Tanzania Prisons.
Bao la kwanza alifunga kwenye mchezo dhidi ya Ken Gold, mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine Mbeya na hilo lilikuwa bao la ushindi ambapo Yanga walisepa na pointi tatu ugenini. Alipachika dakika ya 14 kwa pigo la kichwa akiwa ndani ya 18.
Timu nyingine ambayo ameifunga ni Pamba Jiji ilikuwa Uwanja wa Azam Complex huku Tanzania Prisons ikifungwa mabao mawili na beki huyo wa kazikazi ndani ya kikosi cha Yanga.
Kwa mujibu wa CAF Bacca ameletwa duniani Novemba 12 1997 ni miaka 28 anayo kwa sasa baada ya miaka 10 kwa Neema ya Mungu atafikisha miaka 38 beki wa kazikazi ndani ya kikosi cha Yanga.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.