Watu wawili (2) wamethibitika kuwa na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox nchini Tanzania.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Jenista Mhagama kwenye taarifa kwa umma aliyoitoa Machi 10, 2025 akielezea mwenendo wa ugonjwa huo nchini.
Waziri Mhagama amesema Machi 7, 2025 Wizara ya Afya kupitia mifumo yake ya ukusanyaji wa taarifa na ufuatiliaji wa magonjwa ilipokea taarifa za uwepo wa wahisiwa wenye dalili za vipele usoni, mikononi, miguuni na sehemu nyingine za mwili huku kati yao mhusiwa mmoja ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam.
“Tulichukua sampuli zao na kwenda kuzipima maabara na uchunguzi imethibitishwa kuwa wahisiwa wawili wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha Mpox,” amesema Waziri Mhagama kwenye taarifa yake.
Amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na vituo vyote vya kutolea huduma za Afya, inaendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna wahisiwa wengine ili waweze kupatiwa huduma stahiki.
“Serikali inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika ngazi zote, upimaji wa watu wanaoingia na kutoka kupitia mipaka ya nchi, kuimarisha utoaji wa elimu ya afya na kuhamasisha jamii ili kuwawezesha wananchi kuchuka hatua za kujikinga,” amefafanua Waziri Mhagama.
Aidha Waziri Mhagama amewataka wananchi kuendelea kuzingatia na kutekeleza afua za kujikinga kwa Kuwahi katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu wanapoona mojawapo ya dalili za ugonjwa wa Mpox au kwa piga simu nambari 199 bila malipo; Kuepuka kuchangia vitu kama nguo na matandiko ambavyo vimetumiwa na mtu mwenye dalili za Mpox
Vilevile, wametakiwa kuepuka kugusana kwa kupeana mikono, kubusiana, kukumbatiana au kujamiiana na mtu mwenye dalili za Mpox; Kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili za Mpox na kuepuka kumuhudumia mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox bila kuchukua taharadhari.
Aidha watumishi wa afya wametakiwa kuzingatia kanuni za kujikinga na magonjwa wakati wote wanapowahudumia wagonjwa ikiwemo wenye dalili za vipele na homa; Kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.