AL AHLY YAGOMA KUSHIRIKI MECHI YAO YA DABI DHIDI YA ZAMALEK

Klabu ya Al Ahly ya Nchini Misri imegoma kushiriki mechi yao ya dabi dhidi ya Zamalek inayotarajiwa kuchezwa leo ikisisitiza kuwa Shirikisho la Soka la Misri (EFA) linapaswa kuteua Mwamuzi wa kigeni badala ya kutumia Waamuzi wa ndani pia Klabu hiyo imetishia kujiondoa kwenye Ligi Kuu ya Misri endapo ombi lao halitatekelezwa.

Dabi hiyo ilikuwa sehemu ya hatua ya mbio za ubingwa lakini EFA ilitangaza usiku wa kuamkia leo kuwa mchezo huo utasimamiwa na Waamuzi wa ndani kinyume na makubaliano ya awali na kufuatia mkutano wa dharura uongozi wa Ahly ulitoa tamko rasmi ukitaka mchezo huo uahirishwe hadi Mwamuzi wa kigeni apatikane.

Ahly ilisisitiza kuwa iliwasilisha maombi yake mapema ikitaka Waamuzi wa kigeni kwa mechi muhimu ili kuhakikisha haki inatendeka hasa baada ya makosa ya mara kwa mara ya Waamuzi wa ndani kutotenda haki, hata hivyo Shirikisho ilijibu ikidai muda haukutosha kuwapata Waamuzi wa nje na kuitaka Ahly kuunga mkono Waamuzi wa ndani.

Mpaka sasa EFA haijatoa tamko jipya huku hali ya sintofahamu ikiendelea, yanajiri hayo huku Katika msimamo wa ligi ya Misri Pyramids FC inaongoza kwa alama 42 Ahly ikiwa ya pili na 39 huku Zamalek ikishika nafasi ya tatu kwa alama 32.