BODI YA LIGI YATANGAZA KUAHIRISHA MCHEZO WA DERBY YA KARIAKOO

Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kupitia Kamati yake ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imetangaza kuahirisha mchezo wa Derby ya Kariakoo kati ya wenyeji, Yanga Sc dhidi ya Simba Sc uliopangwa kuchezwa leo Machi 8, 2025 majira ya saa 1:15 usiku katika dimba la Benjamin Mkapa.

Taarifa ya leo Machi 8, 2025 iliyotolewa na TPLB imeeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 34:1(1.3) ya Ligi Kuu kuhusu Kuahirisha Mchezo hatua inayokuja baada ya Simba Sc kuzuiliwa kuingia kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo.

Vilevile TPLB imebainisha kuwa uchunguzi wa matukio kadhaa yaliyoambatana na tukio hilo la klabu ya Simba kushindwa kufanya mazoezi, hauwezi kukamilika kwa wakati hivyo TPLB kupitia Kamati yake ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo huo ili kutoa nafasi ya kupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya maamuzi ya haki.