LICHA YA KUTETEWA NA DROGBA, MOURINHO AFUNGIWA NA TFF KWA UBAGUZI

Meneja wa Fenerbahçe, José Mourinho, amefungiwa michezo minne na kupigwa faini ya jumla ya £35,194 kutokana na kauli alizozitoa za ‘kibaguzi’ baada ya mchezo wa wa debi ya Jiji la Istanbul dhidi ya Galatasaray.

Mourinho alituhumiwa na Galatasaray kwa kutoa kauli za kibaguzi baada ya mchezo huo wa siku ya Jumanne. Hata hivyo Fenerbahçe ilitoa taarifa ikisema kuwa kauli za kocha huyo zilichukuliwa “vibaya kutoka katika muktadha wake”.

Mechi hiyo ya sare ya 0-0 ilichezeshwa na mwamuzi kutoka Slovenia, Slavko Vincic, baada ya vilabu vyote viwili kukubaliana na kuomba achezeshe mwamuzi wa kigeni.

Hata hivyo, mwamuzi wa nne alikuwa Mturuki na Mourinho alirudia tena kutoa lawama zake kuhusu waamuzi wa Kituruki wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mchezo.

Kocha huyo wa Kireno, mwenye umri wa miaka 62, alisema alikwenda katika chumba cha kubadilishia nguo cha waamuzi baada ya mchezo wa Jumatatu, akimwambia mwamuzi wa nne kwamba “kama ungekua mwamuzi, mchezo huu ungekuwa janga kabisa”.

Alhamisi, Shirikisho la Soka la Uturuki (TFF) lilithibitisha kuwa litamchukulia hatua Mourinho kwa masuala mawili tofauti ya kinidhamu.

TFF ilisema itamwadhibu kwa “kauli zake za kudhalilisha na kuudhi kwa mwamuzi wa Kituruki” na kwa kauli za dhihaka na kuudhi kwa jamii ya soka ya Kituruki na waamuzi wa Kituruki”.

Kocha huyo wa zamani wa vilabu vya Chelsea, Manchester United, na Tottenham amepigwa marufuku ya kucheza michezo miwili kuwa uwanjani na amepigwa faini ya 117,000 lira za Kituruki (takriban £2,543).

Mourinho pia amepigwa marufuku ya michezo mingine miwili kwa “kitendo cha kutoupa heshima mchezo” wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mchezo na kupigwa faini nyingine ya £32,651.

Muafrika Didier Drogba, mshambuliaji wa zamani wa Chelsea aliyewahi kufundishwa na mourinho, alimtetea kupitia mtandao wa kijamii kusema kocha huyo si mbaguzi.