VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni ligi namba nne kwa ubora Afrika ikiwa inadhaminiwa na NBC, Yanga wameweka wazi kuwa wanahitaji pointi tatu mbele ya Singida Black Stars.
Huu ni mchezo wa ligi unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC, Complex jioni saa 10:00 ikiwa ni mzunguko wa pili ndani ya 2024/25.
Yanga baada ya kucheza mechi 19 imekusanya jumla ya pointi 49 ikiwa namba moja inafuatiwa na Simba yenye pointi 47 kibindoni baada ya mechi 18.
Ipo wazi kwamba safu ya ushambuliaji ya Yanga ni namba moja kwa timu zenye mabao mengi ikiwa imetupia mabao 48 na kinara ni Clement Mzize mwenye mabao 9 na pasi nne za mabao.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi ameweka wazi kuwa wanatambua mchezo wao utakuwa na ushindani mkubwa lakini wanahitaji kupata pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo.
“Wanaonifahamu wanajua namna gani nina kuwa na uchu wa kupata ushindi, lakini hilo haliondoi ukweli kwamba tunapaswa kuwaheshimu wapinzani ambao tunakutana nao uwanjani.
“Nikisema nawaheshimu wapinzani haimaanishi nina hofu, namaanisha mpira ni mchezo wa ushindani na kila mtu anatumia mbinu mbalimbali kujaribu kushinda hivyo lazima niende kwa tahadhari na umakini hata kama nahitaji kupata alama tatu.”
Singida Black Stars kwenye msimamo ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 37 baada ya kucheza mechi 19 ndani ya msimu wa 2024/25.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.