YANGA KAMILI KUWAVAA COPCO, BAADHI WACHEZAJI WAGONJWA

MABINGWA watetezi wa CRDB Federation Cup Yanga wapo tayari kwa mchezo wao dhidi ya Copco unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC, Complex huku baadhi ya wachezaji wakiwa hawapo fiti kwa mujibu wa benchi la ufundi la timu hiyo.

Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic amesema kuwa wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo huo na wanaamini baada ya kupata ripoti watatambua nani atakuwa tayari kwa ajili ya kutafuta ushindi ndani ya uwanja.

“Hatuna wachezaji 11 tu wenye uwezo na nguvu, tuna wachezaji 25 na tutaweka timu uwanjani ambayo tunaamini inaweza kushinda mchezo wa kesho.

“Tuna baadhi ya wachezaji ambao ni wagonjwa, pia kuna wachezaji waliopata mafua makali na homa. Lakini leo ndiyo siku ambayo tutapata taarifa zaidi na tunatumaini kila mmoja ataweza kurudi.

“Lengo letu kuu bila shaka ni kushinda mechi na pia kushinda Kombe. Ukiwa sehemu ya Young Africans, lengo lako daima ni kushinda kila kitu unachoweza kushinda na hili ndilo lengo letu.

“Tutakutana na timu ambayo tutawaheshimu sana, kama tunavyofanya kila tunapokutana na timu yoyote tunayocheza dhidi yake na tutafanya vivyo hivyo na tutajaribu kushinda mechi kwa kila tunachoweza ili tuweze kusonga mbele.”