SIMBA LICHA YA USHINDI KAZI BADO HAIJAISHA

IKIWA ugenini Januari 5 2025 Simba ilisepa na ushindi wa bao 1-0 na kukomba pointi tatu mazima kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.

Ni Jean Ahoua kiungo wa Simba alifunga bao pekee katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya SC Sfaxine dakika ya 34 akitumia pasi ya Leonel Ateba.

Kipindi cha kwanza kilitosha kwa Simba kumaliza kazi huku kipindi cha pili wakiingia kwa mbinu kubwa ya kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo hayakuleta matokeo chanya kwa upande wao na ulinzi uliimarika licha ya makosa kutokea katika dakika za lala salama ambapo Simba waliruhusu kona na faulo eneo la hatari.

Mshambuliaji Ateba alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 45 akiungana na Ellie Mpanzu ambaye alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 27. Ikumbukwe kwamba ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Mpanzu kwenye anga la kimataifa alikwama kumaliza dakika zote 90 nafasi yake ilichukuliwa na Mavambo.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa licha ya ushindi bado hawajamaliza kazi kwa kuwa kuna mechi nyingine zinafuata na mpango ni kuona wanapata pointi tatu muhimu.

“Tumeshinda ugenini hii ni furaha kwetu lakini bado hatujamaliza tuna kazi nyingine yakufanya kwenye mechi zinazofuata ili kupata ushindi na malengo ni kutinga hatua ya robo fainali.”

Kwenye Kundi A Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 9 baada ya kucheza mechi 4 vinara ni Costantine wakiwa na pointi 9 hawa waliifunga Simba bado kazi inaendelea kwa timu tatu kusaka nafasi ya kutinga robo fainali kwa kuwa Bravos iliyopo nafasi ya tatu ina pointi 6 ina nafasi ya kutinga robo fainali huku CS Sfaxine mwendo ameumaliza akiwa hajakusanya pointi baada ya kucheza mechi nne.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.