Shirikisho la soka Afrika (CAF) limetangaza kuwa droo ya michuano ya CHAN 2024 itafanyika nchini Kenya, huku kukiwa na shaka juu ya uenyeji wa michuano hiyo nchini humo.
Michuano hiyo inayozikutanisha timu za taifa kwa upande wa wachezaji wanaocheza ligi za ndani, imepangwa kufanyika kuanzia tarehe 1 hadi 28 Februari 2025 katika nchi za Kenya, Tanzania na Uganda.
Maandalizi yanaendelea huku nchi nyingine zikiwa tayari zimepokea viwanja na vifaa vingine vyote muhimu vimekamilika isipokuwa Kenya ambayo bado haijakamilisha ukarabati wa viwanja hivyo.
Katika taarifa iliyotolewa Januari 5, 2025, CAF ilithibitisha kwamba droo ya CHAN 2024 itafanyikia Nairobi, katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Kenyatta (KICC) Januari 15, 2025.”
Zikiwa zimesalia siku 28 kabla ya michuano hiyo kuanza, CAF bado haijatangaza timu nyingine mbili zaidi ambazo zitaungana na nyingine 17 ambazo zimeshafuzu.