VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Simba wamepotezwa na Yanga kwenye upande wa mabao ya kufunga ambapo wameachwa kwa bao moja tu baada ya wote kucheza mechi 15.
Katika mechi tano za Sead Ramovic kwenye ligi ni mabao 18 Yanga imefunga huku ikiandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kupata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Fountain Gate ikiivunja rekodi ya Kagera Sugar 2-5 Simba ambao huu ni ushindi mkubwa wa kwanza kupatikana ndani ya ligi rekodi iliyoandikwa na Simba.
Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ni mabao 31 wamefunga ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 huku Yanga wakiwa wamefunga jumla ya mabao 32.
Ni tofauti ya bao moja inawafanya Yanga kuwa namba moja kwenye timu ambazo zimefunga mabao mengi kwenye mechi za ushindani.
Wakati Yanga ikiwa namba moja kwenye upande huu, Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 40 huku Yanga nafasi ya pili na pointi 39.
Katika mabao ya kufungwa, Yanga imefungwa mabao sita na Simba imefungwa mabao matano ikiwa ni timu inayoongoza kwa kufungwa mabao machache.
Fountain Gate ni namba moja kwa timu ambazo zimeruhusu mabao mengi uwanjani ambayo ni 32 baada ya kucheza mechi 16 ipo nafasi ya sita kwenye msimamo.