HAJI MANARA ATIBUA, AONYWA NA JESHI LA MAGEREZA

JESHI la Magereza Tanzania limemuonya Mwanachama wa klabu ya Yanga Sc, Haji Sunday Manara kwa kauli isiyo ya kiungwana yenye viashiria vya kutweza utu na yenye mwelekeo wa kulifedhehesha Jeshi hilo aliyotoa baada ya mchezo kati ya Yanga Sc dhidi ya Wajelajela, Tanzania Prisons katika dimba la KMC Complex.

Taarifa ya leo Desemba 23 iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Magereza, SACP. Elizabeth Mbezi imebainisha kuwa baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Ndugu Haji Manara alianza kuongea na Vyombo vya Habari akiwa ameegesha gari lake mbele ya gari la Jeshi la Magereza.

“Kwa kuwa alikuwa amezuia gari la Jeshi kuondoka, aliombwa atoe nafasi kwa kusogeza gari lake kuruhusu gari alilokuwa amelizuia liweze kupita na yeye aendelee na mahojiano yake.”——imesema taarifa hiyo

“Hata hivyo, pamoja na kuombwa alikataa kwa dharau na kuanza kutoa maneno yasiyo ya kiungwana, yenye viashiria vya kutweza utu na yenye mwelekeo wa kulifedhehesha Jeshi la Magereza.”

“Uongozi wa Jeshi unatoa onyo na kuwataka wananchi kuacha kutoa kauli zenye mwelekeo wa kubeza, kutweza, kudharau mamlaka yake au kulifedhehesha na kwamba halitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayehusika.”——imesema