WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye anga la kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa hatua ya makundi wanatarajiwa kuwa kazini leo saa 1:00 usiku (kwa saa za Afrika Mashariki) katika mchezo wa mzunguko wa pili Kundi A Kombe la Shirikisho dhidi ya CS Constantine mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Chahid Hamlaoui nchini Algeria.
Timu zote mbili zimejikusanyia alama 3 katika michezo yao iliyopita katika kundi hilo, Simba waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bravos ya Angola huku Constantine wakiishinda mchezo wao wa kwanza ugenini dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia kwa bao 1-0.
Wenyeji wa mchezo huo, CS Constantine wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Algeria, Ligue 1 wakiwa na alama 19 katika michezo 11 msimu huu, huku wakipoteza mchezo mmoja tu kati ya michezo yao mitano ya mwisho, wakishinda jumla ya michezo mitatu na kutoa suluhu mchezo mmoja, wakifunga jumla ya mabao matano na kuruhusu mabao matatu.
Simba ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania wakiwa na alama 28 katika michezo 11 wakiwa na ushindi wa asilimia 100 katika michezo mitano ya mwisho wakishinda michezo yote wakifunga jumla ya mabao 10 bila kuruhusu bao kwenye mechi hizo za ushindani.
Aidha, katika mchezo mwingine wa kundi hilo, FC Bravos ya Angola itakuwa nyumbani kuwakaribisha CS Sfaxien ya Tunisia, huku timu zote zikitafuta ushindi wa kwanza katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa saa 1:00 kwa saa za Afrika Mashariki.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema kuwa wanamchezo mgumu dhidi ya wapinzani wao hivyo watapambana kupata matokeo chanya katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.