WATUMISHI wa magereza wameshauriwa kuwekeza kwa busara katika sekta mbalimbali wakiwa bado kazini, ili kujihakikishia maisha mazuri na endelevu baada ya kustaafu.
Ikumbukwe kwamba kuna uwekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na michezo ambayo wapo wamiliki wa maduka ya vifaa vya michezo wanatengeneza mkwanja humo huku wakiwa wanaendelea na kazi pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji.
Rai hiyo ilitolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Bwana Moses Magogwa, wakati wa hafla ya kumuaga Kamishina Msaidizi wa Magereza, ACP George Stone Msumule, aliyehitimisha utumishi wake rasmi tarehe 1 Desemba 2024.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa hafla hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Magereza Kibaha, Magogwa aliwahimiza watumishi kujiandaa mapema kwa kuhakikisha wanapata makazi bora, kusomesha watoto, na kuwekeza katika sekta zenye tija kama ardhi na mifuko ya uwekezaji.
“Ni muhimu kujiandaa kwa maisha baada ya kustaafu kwa kuwa na rasilimali zitakazowezesha maisha ya heshima na uhuru wa kiuchumi. Hili linaweza kufanikishwa kupitia nidhamu ya kifedha, kuwekeza katika elimu ya watoto wetu, na kushiriki shughuli za maendeleo.” amesema Magogwa.
Aidha, aliwakumbusha watumishi wa magereza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, nidhamu, na uaminifu, akisisitiza kuwa hiyo ndiyo njia ya kulinda maslahi ya taifa na kujenga uaminifu wa wananchi. Pia aliwataka kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika juhudi zake za kuleta maendeleo.
Katika risala yake, ACP George Stone Msumule alitoa shukrani kwa Jeshi la Magereza kwa kumpa fursa ya kutumikia taifa kwa muda mrefu. Alieleza kuwa utumishi wake umekuwa wa manufaa makubwa kwake binafsi na kwa jamii, akiahidi kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo, kutunza mazingira, na kudumisha amani katika jamii anayoishi.