>

YANGA HESABU NDEFU KIMATAIFA, MGENI RASMI ANATOKA CAF

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa hesabu kubwa ni kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O ya Burundi kwenye mchezo wa marudiano.

Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kwenye mchezo wa awali uliochezwa Azam Complex wakiwa wageni waliibuka na ushindi wa mabao 4-0 wanakibarua kingine leo Agosti 24 kusaka ushindi wa jumla kwenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Gamondi amesema: “Tunajiamini na matokeo tuliyopata mechi iliyopita lakini bado tunaheshimu kuwa tuna dakika 90 nyingine za kupambana, kipaumbele chetu ni kufuzu hatua inayofuata. Tunatambua kwamba utakuwa mchezo wenye ushindani ila tupo tayari.”

Kwa upande wa Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema: “Tumeweka rekodi ya kwanza ya klabu kufanya mkutano mkubwa wa CAF, tunazungumzia ukumbi na sio chumba. Jambo hili ni heshima kubwa sana kwetu, kimsingi tumeheshimisha soka la Tanzania.

“Tunawaalika sana Chamazi kutakuwa na burudani kubwa sana, tutakuwa na DJ Ally B pamoja na wasanii mbalimbali ambao tutawatangaza. Kwahiyo tujitahidi kadiri iwezekanavyo tuwahi kukata tiketi mapema sana.

“Nitumie fursa hii kuwatangazia mgeni rasmi ambaye atakuwepo kwenye uzinduzi, ni mjumbe wa kamati ya CAF na Mwenyekiti wa vilabu Afrika, ambaye ni Injinia Hersi Said.”