>

KUMBE! SIMBA WANASHINDA LAKINI HAWANA FURAHA

AHMED Ally, meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa wanashinda lakini hawana furaha kwa kuwa bado wanatengeneza timu hiyo.

Mchezo wa kwanza wa Simba katika Ligi Kuu Bara ilikuwa dhidi ya Tabora United uliochezwa Uwanja wa KMC, baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 3-0 Tabora United kwa msimu wa 2024/25 ambao una ushindani mkubwa.

Mabao yalifungwa na Che Malone dakika ya 14, Valentino Mashaka dakika ya 67 na Awesu Awesu dakika ya 90. Che Malone ambaye ni beki alichaguliwa kuwa mchezaji bora kwenye mchezo huo.

Ally amesema: “Tunashinda lakini hatuna furaha kwa kuwa ushindi ambao tunapata unatokana na juhudi za wachezaji binafsi bado timu haijawa kwenye muunganiko mzuri kwa kuwa wachezaji wengi ni wageni licha ya uwezo ambao wanao.

“Tulipomaliza mchezo dhidi ya Tabora United tumeanza maandalizi kuelekea mchezo ujao dhidi ya Fountain Gate tunahitaji kupata ushindi na timu icheze vizuri pia. Hilo linawezekana kwa kuwa wachezaji wanajituma na makosa yaliyopita yanafanyiwa kazi. Kuanza kwa ushindi kwenye mchezo wa kwanza ni mwanzo mzuri.”

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Agosti 25 2024, Uwanja wa KMC, Mwenge utakuwa ni mchezo wa pili kwa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.