>

YANGA KUWAKABILI VITAL’O UWANJA WA MKAPA KWA TAHADHARI

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa utawakabili wapinzani wao Vital’O Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa tahadhari kubwa kwa kuwa bado hawajatimiza malengo licha ya kupata ushindi kwenye mchezo wa kwanza.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Azam Complex Agosti 17 2024 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Vital’O 0-4 Yanga mabao yakifungwa na Prince Dube, Clatous Chama, Clement Mzize na Aziz Ki.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa wanatambua mchezo wao utakuwa mgumu hivyo wanafanya maandalizi mazuri kupata matokeo chanya.

“Ulikuwa ni ushindi mzuri kwetu lakini haujatupeleka pale ambapo tulikuwa tunakataka kwenda. Mechi ya kwanza ilikuwa ni nzuri na tunaamini kwamba wapinzani wetu Vital’O watakwenda kufanyia kazi makosa ambayo yalitokea kwenye mchezo wetu wa marudiano.

“Tumechagua Uwanja wa Mkapa Agosti 24 ili kutafuta ushindani kwenye mchezo wetu na utakumbuka kwamba kuna wakati tulicheza na Djibout palepale Uwanja wa Azam Complex ila hii itakuwa ni mechi yetu tutacheza Uwanja wa Mkapa saa 1:00 usiku.

“Kutokana na CAF kwa yale waliyoyaona kwenye kilele cha Wananchi kuujaza Uwanja wa Mkapa na Uwanja wa Uhuru,CAF wameturuhusu tufanye uzinduzi rasmi Uwanja wa Mkapa na hii ni heshima kwetu tunakwenda kwenye mchezo huu kutuma ujumbe mzito barani Afrika.”