>

YANGA YAWATULIZA WAPINZANI WAO, 4G YASIMIKWA

VITAL’O ya Burundi imepoteza mchezo wake wa awali dhidi ya Yanga Uwanja wa Azam Complex baada ya dakika 90 kugota mwisho mazima.

Ubao umesoma Vital’O 0-4 Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi ambaye alianza na Clatous Chama, Aziz Ki, Prince Dube kwenye orodha ya wachezaji wa kikosi cha kwanza.

Kazi ilianza kipindi cha kwanza kwa Yanga kupata bao la uongozi na kuwafanya waendele vyumba vya kubadilisha nguo wakiwa wanaongoza kwa bao hilo lilifungwa dakika ya 6 na muuaji anayetabasamu Prince Dube.

Kipindi cha pili Yanga iliongeza bao la pili kupitia kwa Clatous Chama dakika ya 67 hiyo ni baada ya wapinzani wao kuwa kwenye hesabu za kuweka usawa bao walilofungwa wakiwa wanatafuta njia wakafungwa bao la pili.

Ilikuwa ni shuti la Aziz Ki ambalo liligonga mwamba na kurejea uwanja akiwa kwenye utulivu Chama alipiga shuti kwa mguu wake wa kushoto ambalo lilizama nyavuni mazima na kumshinda mlinda mlango wa Vital’O.

 Clement Mzize hakukata tamaa aliendelea kutimiza majukumu yake na alisepa na kijiji chake mpaka akafunga bao la tatu ilikuwa dakika ya 74.

Msumari wa nne kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika umepachikwa na Aziz Ki dakika ya 90 kwa pigo la penalti. Hivyo dakika 90 zimekamilika Yanga wameibuka na ushindi kwenye mchezo wa hatua ya awali.