Baba wa nyota wa soka wa Uhispania Lamine Yamal mwenye umri wa miaka 17 ameripotiwa kuchomwa kisu mara kadhaa kwenye eneo moja la maegesho ya magari.
Kulingana na ripoti katika vyombo vya habari vya Uhispania, Mounir Nasraoui alishambuliwa katika mji wa pwani wa Mataró, kaskazini mwa Barcelona, Jumatano usiku na kundi la watu aliozungumza nao mapema mchana.
Polisi wa Catalonia wamethibitisha kuwa takriban watu watatu wamekamatwa, shirika la habari la AFP linaripoti.
Bw Nasraoui alipelekwa hospitalini mjini Barcelona akiwa katika hali mbaya lakini sasa anasemekana kuwa yuko sawa.
Shambulio hilo lilifanyika karibu na kitongoji cha Rocafonda ambapo Yamal alikulia.
Mapema siku hiyo, Bw Nasraoui inasemekana aligombana na kundi la watu aliokutana nao alipokuwa akimtembeza mbwa wake, gazeti la Uhispania El Pais liliripoti.
Saa kadhaa baadaye, alifikiwa na kundi lile lile kwenye maegesho ya magari na kuchomwa kisu “mara kadhaa”.Sababu ya kuchomwa kisu haijajulikana kwa sasa.Ripoti kwenye tovuti ya michezo ya Relevo ilisema kuwa Bw Nasraoui alitarajiwa kusalia hospitalini kwa siku mbili au tatu chini ya uangalizi.
Lamine Yamal, mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea nchini Uhispania, alishiriki michuano ya Euro 2024 ambapo alitajwa kuwa Mchezaji Chipukizi bora wa Mashindano hayo.
Winga huyo alitoa pasi iliofungwa na Nico Williams likiwa, bao la ufunguzi wakati Uhispania ilipoilaza England 2-1 kwenye fainali iliyochezwa Berlin.
Muda mfupi baada ya Uhispania kunyanyua kombe hilo, mashabiki walijipanga katika mitaa ya Mataró wakimshangilia nyota wao mchanga.
Baada ya kukulia katika mji huo, Yamal alitumia baadhi ya miaka yake ya ujana katika chuo kikuu cha Barcelona cha La Masia.