GAMONDI AWAPA TANO MASTAA WAKE

MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amewapa tano mastaa wake ikiwa ni pamoja na Clement Mzize, Duke Abuya, Dickson Job kwa kushirikiana kuanza na taji la Ngao ya Jamii kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa Mkapa dhidi ya Azam FC.

Katika mchezo huo uliochezwa Agosti 11 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 4-1 Azam FC ambapo bao la utangulizi kwa Azam FC lilifungwa na kiungo mshambuliaji Feisal Salum ilikuwa dakika ya 13 na Yanga waliweka usawa kupitia kwa Prince Dube aliyetumia pasi ya Mudathir Yahya.

Gamondi amebainisha kuwa wachezaji wote wamekuwa wakicheza kwa ushirikiano mkubwa kwenye mechi zote jambo ambalo ni muhimu na linawapa ushindi licha ya kuwa na ushindani mkubwa kwenye mechi ambazo wanacheza.

“Pongezi kubwa kwa wachezaji namna ambavyo wamekuwa wakijituma kutimiza majukumu yao hili ni kubwa na inafurahisha kuona kwamba tunapata matokeo ni muhimu kuwa na mwendelezo mzuri.

“Tulianza kufungwa kwenye mchezo wetu wa fainali ila tulitulia na kutambua kwamba bado tuna nafasi tukatengeneza na kuzitumia kwa kuwa tulifanya vizuri pongezi wanastahili wachezaji na ni furaha kuanza kwa kutwaa taji kwenye msimu mpya.”

Azam FC na Yanga zitapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo zote zitaanzia hatua ya awali.