AZAM FC: TULIKUWA BORA LICHA YAKUPOTEZA FAINALI

UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kwamba licha yakupoteza mchezo wao wa fainali mbele ya Yanga bado walikuwa kwenye ubora katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Agosti 11 2024.

Ipo wazi kuwa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu,Miguel Gamondi ilitwaa ubingwa huo kwa ushindi wa mabao 4-1 katika fainali iliyokuwa na ushindani mkubwa.

Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC ameweka wazi kuwa wanatambua namna kazi kubwa ilivyokuwa kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ndani ya dakika 90.

“Ilikuwa kazi kubwa kwa kila mchezaji ndani ya uwanja lakini tunakwenda kuona namna gani tunakwenda kuwa bora. Mchezo wetu wa fainali dhidi ya Yanga tulikuwa bora kwenye uwanja na hilo lipo wazi hivyo tunakwenda kufanyia kazi makosa yaliyopita.

“Waliokuwa nyumbani wameona kwamba kila mchezaji alikuwa anacheza kwa juhudi na Feisal Salum ameshinda mechi yake dhidi ya Yanga na kukamilisha kazi yake uwanjani licha ya kwamba tumepoteza mchezo wetu wa fainali bado tupo imara. Timu bora imepoteza mbele ya timu ambayo haikuwa bora.”