YANGA KULIPA KISASI KWA MKAPA

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa kuelekea kwenye kilele cha Wiki ya Wananchi Agosti 4 2024 watalipa kisasi cha mtani wao wa jadi Simba kwa kuonyesha ukubwa walionao kwa kuujaza Uwanja wa Mkapa.

Ipo wazi kwamba Agosti 3 2024 ilikuwa ni Simba Day ambapo mashabiki wa Simba walijitokeza wengi na mapema kabla ya tukio ilitagazwa kuwa tiketi zote zimeuzwa hivyo ilikuwa ni Full House Uwanja wa Mkapa.

Baada ya tamasha la Simba kugota mwisho kwa burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii ikiwa ni pamoja na King Kiba, Joh Makini mchezo wa kimataifa wa krafiki dhidi ya APR ambapo Simba ilishinda mabao 2-0 watupiaji wakiwa ni Deborah Fernandes na Edwin Balua leo ni kilele cha Wiki ya Wananchi.

Ali Kamwe, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga usiku wa kuamkia Agosti 4 2024 alikuwa Uwanja wa Mkapa na kubainisha kwamba wanakwenda kuonyesha maana halisi ya Full House.

“Wameanza wenyewe sasa sisi tunakwenda kumaliza tunataka kuandika rekodi ikifika saa sita mchana mageti ya Uwanja wa Mkapa yafungwe maana tumeona wenzetu mpaka saa 10 jioni bado mageti yalikuwa wazi lakini sisi tunakwenda kuandika rekodi ambapo tutatumia na Uwanja wa Uhuru pia.”

Kwenye Wiki ya Wananchi Yanga inatarajia kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Red Arrows ambao ni mabingwa wa Kagame Cup.