KIBU KUKUTANA NACHO HUKO SIMBA

UONGOZI wa Simba umebainisha kuwa kiungo Kibu Dennis atapewa adhabu ili kuwa fundisho kwa wachezaji wengine ndani ya timu hiyo kuwa na nidhamu.

Ikumbukwe kwamba Kibu hakuwa na timu kambini nchini Misri na taarifa kutoka Simba zilibainisha kwamba alikuwa akitoa sababu tofauti tofauti alipojulishwa kwamba anatakiwa kuripoti kambini.

Mpaka kambi inakamilika nchini Misri Kibu hakuwa sehemu ya kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ambaye alikuwa akiwapa mbinu wachezaji wa Simba itakayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa tayari Kibu amerejea baada ya kuwa Ulaya kwa muda lakini atachukuliwa hatua kutoka kwenye taasisis hiyo ya Simba.

“Kibu alikuwa akitafuta malisho mengine nje lakini hakufuata utaratibu na tayari amerejea na kuzungumza na kocha kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake hivyo yupo Simba kwa kuwa ana mkataba na timu.

“Kwa ambacho kimetokea atachukuliwa hatua ili kuwa funzo kwa wengine kwa kuwa hii ni taasisi na ina taratibu zake kwenye kuendesha majukumu.”.

Kibu mkataba wake aliongeza wa miaka miwili kwa mujibu wa Simba hivyo yupo hapo mpaka 2026 akitimiza majukumu yake.