MATAJIRI wa Dar Azam FC Agosti 3 2024 wanatarajiwa kuwa kazini kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.
Mchezo huu ni maalumu baada ya Azam FC itakayopeperusha bendera ya Tanzania Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kupewa mualiko kwenye kilele cha siku ya Rayon Sports Day.
Ni Agosti 2 kikosi cha Azam FC kiliwasili Rwanda na usiku kilifanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuivaa Rayon Sports.
Yusuph Dabo, Kocha Mkuu wa Azam FC amesema kuwa wanaamini watakuwa na mchezo mzuri mbele ya wapinzani wao ambao wapo imara.
“Tunatarajia kuwa na mchezo mzuri dhidi ya wenyeji wetu ambao wametualika, ni sherehe yao nasi tutafanya sherehe yetu uwanjani kwa kucheza mchezo mzuri.”
Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki, utachezwa Uwanja wa Pele Kigali, leo Jumamosi saa 1.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Azam FC ni Feisal Salum ambaye mkononi ana tuzo ya MVP wa CRDB Cup, Yannick Bangala.