MASHABIKI WA YANGA WAGAWA MAHITAJI MBALIMBALI KWA WAFUNGWA KATIKA GEREZA LA ISUPILO

MASHABIKI wa Tawi la Yanga Mjini Mafinga huko Iringa, wametoa huduma ya kuwakarimu wahitaji na waishio katika mazingira magumu wakiwemo Watoto yatima pamoja na kuwatembelea wafungwa katika Gereza la Isupilo Wilayani Mufindi.

Mashabiki hao wamegawa mahitaji mbalimbali kwa wafungwa katika Gereza la Isupilo ikiwemo mafuta ya kupikia , Sabuni miche 75, Karanga debe moja na fedha tasilimu.

Sanjari na hayo, Mashabiki hao wamewafikia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kituo cha familia ya Yuresalemu Ihongole na kugawa baadhi ya mahitaji ikiwemo nguo za watoto wakike na wakiume, sukari kg50, Sabuni pamoja na vyakula.

Akizungumza Mwenyekiti wa Tawi la Yanga Mjini Mafinga Hosea Mwambene amesema wamekuwa na desturi hiyo kila mwaka kwa kufanya sherehe inayoambatana na kutoa mahitaji mbalimbali ili kuendelea kuongeza wigo mpana wa furaha katika Klabu yao.

Aidha, Mwenyekiti Mwambene ametoa wito kwa wapenzi na washabiki wa Yanga kujiunga na Tawi hilo ili kuwa Wanachama hai.