>

HUYU HAPA CEO MPYA SIMBA

RASMI uongozi wa Simba umemtangaza Uwayezu Francois Regis raia wa Rwanda kuwa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo kuanzia Agosti 1, 2024 mara mkataba wa Imani Kajula ambaye yupo kwenye nafasi hiyo kwa sasa kugota mwisho.

Taarifa iliyotolewa na Simba mapema Julai 26 kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohamed Dewji, (Mo) imeeleza kuwa wameridhia ombi la Kajula kutoendelea na nafasi hiyo kama ambavyo ameomba hivyo wanamtangaza CEO mpya atakayechukua mikoba yake muda wake utakapogota mwisho.

Uwayezu alikuwa Makamu Mwenyekiti wa APR ya Rwanda na tayari ameagwa na viongozi wa klabu hiyo hivyo yupo huru kuanza majukumu yake mapya na timu hiyo ambayo itashiriki Kombe la Shirikisho msimu wa 2024/25.

Ikumbukwe kwamba Kajula alitambulishwa rasmi Januari 26 2023 alichukua mikoba ya Barbra Gonzalez aliyebwaga manyanga Desemba 10 2022. Julai 15 2024 taarifa ilitolewa na uongozi wa Simba kwamba wameridhia ombi lake la kuomba kutoongeza mkataba.

Awali ilikuwa inatajwa kuwa pengine Barbra angerejeshwa kwenye nafasi hiyo kwa mara nyingine tena lakini haijawa hivyo baada ya CEO mpya kutangazwa.