UONGOZI wa Yanga umebainisha kwamba utakwenda Afrika Kusini kwa ajili ya mwendelezo wa maandalizi ya msimu wa 2024/25 wakiwa wamealikwa kutokana na thamani ya timu hiyo kupanda.
Chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi, Yanga msimu wa 2023/24 iliweka kambi Bongo na ikafanikiwa kutwaa taji la ligi ikimaliza msimu ikiwa na pointi 80 baada ya kucheza jumla ya mechi 30.
Mbali na taji la ligi ilitwaa CRDB Federation Cup kwa ushindi dhidi ya Ihefu kwenye mchezo wa fainali kwa sasa ipo Bongo ikiendelea na maandalizi kuelekea msimu mpya unaotarajiwa kuanza Agosti 16.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kwamba watakuwa tofauti kwa msimu wa 2024/25 kwenye upande wa kambi baada ya kupata mialiko kutoka sehemu mbalimbali wakaamua kwenda Afrika Kusini.
“Klabu yetu inaendelea na mazoezi pale AVIC TOWN kwa ajili ya Pre Season. Baada ya thamani yetu kupanda, tumepata mwaliko wa kushiriki mashindano maalumu. Tumealikwa pale Afrika Kusini kwenye mashindano ya Toyota Cup na mashindano ya TS Galaxy.
“Safari kuelekea Afrika Kusini inatarajiwa kuwa Julai 18 kisha tutacheza mechi zetu huko tukimaliza tunatarajia kurejea Julai 30 Dar kwa maandalizi ya mwisho kuelekea kwenye Wiki ya Mwananchi.”